WAZIRI JAFO ATOA SIKU SABA KWA MTENDAJI MKUU WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUANZA KUTEKELEZA UJENZI WA MRADI WA ULIOKUWA UMEKWAMA

Naibu Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo akisalimiana kwa kumpa mkono mmoja wa wagonjwa mara alipofanya ziara yake ya kushtukiza katika hospitali ya tumbi kwaa ajili ya kuweza kufanya ukaguzi katika mradi wa upanuzi wa hospitali hiyo.PICHA NA VICTOR MASANGU


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 

NAIBU Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa Tumbi na kutoa muda wa wiki moja kwa mtendaji mkuu wa Shirika la elimu Kibaha kuanza mara moja ujenzi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa majengo baada ya kubaini umekwama kwa kipindi cha miaka saba bila ya kuendelezwa kitu chochote hali ambayo imesababisha kwa sasa eneo hilo kuota nyasi na kugeuka kuwa vichaka.

Jafo akizungumza kwa masikitiko makubwa na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Tumbi,pamoja na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amechukizwa kuona mradi huo kutelekezwa na kusababisha miundombinu yake ya majengo kuchakaa kabla hata ya kuanza kutumika kitendo ambacho amekilaani vikali na kusema suala hilo hawezi kulifumbia macho hata kidogo.

Jafo alibainisha kuwa serikali tayari imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 600 na fedha hiyo imeshaingizwa katika Ofisi ya Ras Pwani tangu mwaka jana kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo lakini anashangazwa kuona mradi huo kusimama, hivyo amewaagiza watendaji wa mamlaka zinazohusika kukutana na kuliweka sawa jambo hilo kwa lengo la kuweza kuboresha sekta ya afya.

“Kwa kweli natoa wiki moja kwa mtendaji mkuu kufanya haraka iwezeknavyo mradi huu wa upanuzi ambao ulikuwa umesimama kwa kipindi kirefu kukaa chini na watendaji wenzake wakubaliane na kuweza kuanza mara moja ujenzi huo maana fedha zipo tu na kwamba tayari tumeshazitoa shilingi milioni 600 sasa sijui nini tatizo kwa hiyo wiki ijayao nataka kuona ujenzi huo unaanza kuendelea,”alisema Jafo.

Aidha Jafo alisema kwamba lengo kubwa la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kwamba inaboresha huduma ya matibabu kwa wananchi wote hivyo asingependa kuona baadhi ya watu wanarudisha nyuma juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.

Kutokana na agizo hilo la Naibu Waziri mwandishi wa habari hizi aliweza kubisha hodi na kuweza kuzungumza na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa shirika la elimu Kibaha Robert Shilingi amebainisha kuwa vikwazo na changamoto kubwa zinazopelekea kukwama kwa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa hospitali ya Mkoa ya Tumbi ni ukata wa fedha ambao ulikuwa unawakabili hivyo kupelekea ujenzi kutokamilika kwa wakati.

Naye Kaimu afisa miliki wa shirika la elimu Kibaha Injinia Zacharia Mwinuka ambaye pia ndiye alikuwa anasimamia ujenzi amesema kwamba mradi huo wa upanuzi ulianza tangu mwaka 2009 na kufafanua zaidi sababu nyingine ni kuwepo kwa ufinyu wa bajeti pamoja na ucheleweshwaji wa fedha kutoka serikalini.

MRADI huo wa ujenzi kwa ajili ya upanuzi wa hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa Tumbi ulianza utekelezaji wake tangu mnamo mwaka 2009 na ulitarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miaka mitatu lakini hadi kufikia mwaka huu wa 2017 bado haujamalizika na miundombinu yake ya majengo tayari imeshaanza kuchakaa licha ya serikali ya awamu ya tano kutoa kiasi cha shilingi 600 kwa ajili ya ujenzi huo.

Comments

Popular posts from this blog

JUHUDI ZA MWALIMU NYERERE KATIKA KUKUZA NA KUIMARISHA SEKTA YA UTALII NCHINI